Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Imam Sajjad (a.s.) anamwomba Mwenyezi Mungu kupitia maneno haya yenye maana kubwa:
«اللَّهُمَّ ... اسْتَعْمِلْنِی بِمَا تَسْأَلُنِی غَداً عَنْهُ»
Ewe Mola! Nitumikishe katika mambo ambayo kesho Siku ya Kiyama utanihesabia kwayo. (1)
Sherehe:
Dua hii, ambayo pia imepokewa kutoka kwa Bibi Fatima Zahra (a.s.) na Imam Sadiq (a.s.), ni taa ya mwongozo kwa kila mtu, hasa kwa vijana na wanafunzi wa dini wanaotamani kuanza maisha ya kumuabudu na kumtii Mwenyezi Mungu.
Mwanadamu katika maisha hupitia njia nyingi na fursa tofauti. Kupitia dua hii tunamwomba Mola wetu atuongoze ili mapenzi yetu, vipaji vyetu, uwezo wetu na nafasi tulizonazo ziwe katika njia inayompendeza Yeye. Kwa maneno mengine, tunamwomba Mwenyezi Mungu azielekeze nguvu na akili zetu katika njia ya kumtumikia Yeye.
Imam Ali (a.s.) katika Dua ya Kumayl anamwomba Mola kupitia maneno haya:
«یَا رَبِّ يا رب يا رب، قَوِّ عَلی خِدْمَتِکَ جَوارِحِی، وَاشْدُدْ عَلَی الْعَزِیمَةِ جَوانِحِی»
Ewe Mola wangu! Vitie nguvu viungo vyangu katika kukutumikia wewe, na uimarishe azma na dhamira yangu katika kukutii. (2)
Kwa tafsiri ya kisasa, Imam Ali (a.s.) anatuombea tuweke “vifaa vyote vya kimaumbile na kiroho” kwenye kumtumikia Mwenyezi Mungu – yaani akili, mwili, muda na nguvu zote ziwe katika njia ya ibada.
Mwisho kabisa, maneno ya Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) yanajumlisha maana zote hizi:
«اَللَّهُمَّ لاَ تَکِلْنِی إِلَی نَفْسِی طَرْفَةَ عَیْنٍ أَبَداً»
Ewe Mola! Usiniachie hata kwa muda wa kupepesa jicho nijitegemee mwenyewe. (3)
Rejea:
1- Sahifa Sajjadiyya, dua ya ishirini – Dua ya Makarimul-Akhlāq
2- Dua ya Kumail
3- Al-Manāqib, juzuu ya 1, uk. 57
Imeandaliwa na Idara ya Elimu na Utamaduni ya Shirika la Habari la Hawza.
Maoni yako